Serikali ya kaunti ya Taita Taveta imesema itaongeza mashine za kusafisha figo katika hospitali ya mpakani ya Taveta.
Akizungumzia hilo katika hafla ya kuadhimisha siku ya ugonjwa wa figo ulimwenguni mjini Taveta, waziri wa afya katika kaunti hiyo Daktari Gifton Mkaya amesema ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu husababisha figo kuathirika zaidi.
Mkaya amesema mashine hizo zitakuwa zenye manufaa mengi kwani wagonjwa wengi hutumwa kwenye hospitali ya Moi mjini Voi na wengine katika hospitali kuu ya kanda ya pwani kaunti ya Mombasa.
Vilevile, amewataka wenyeji kufika hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa figo ili kupata tiba kwa wakati ufaao.
Wakati huohuo amewahimiza wenyeji na wakenya kwa jumla kula vyakula vya kiasili ili kudhibiti kuugua magonjwa mbalimbali.
Haya yanajiri huku madaktari wakilalamikia uhaba wa mkubwa wa mashine za kusafisha damu kwenye hospitali nyingi nchini huku Daktari mkuu anayeshughulikia ugonjwa wa Figo Daktari Mathew Koech akisema kati ya wagonjwa zaidi milioni Moja ambao wanahitaji mashine hizo ni wagonjwa elfu 50 pekee ambao wananufaika.
SERIKALI YA KAUNTI YA TAITA TAVETA KUONGEZA MASHINE ZA KUSAFISHA FIGO

