Zaidi ya wanafunzi mia nane katika wadi ya Ganda eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi, wamenufaika na kima cha shilingi milioni 4.85, fedha za basari kutoka kwa serikali ya kaunti ya Kilifi.
Kulingana na mwakilishi wadi hiyo Oscar Wanje, ni kuwa wanafunzi hao ni pamoja na wale wa shule za upili, vyuo vikuu pamoja na vile vya kiufundi na kuongeza kuwa idadi kubwa ya wanafunzi katika eneo hilo, hawakuwa wamejiunga na kidato cha kwanza kutokana na ukosefu wa karo, ila sasa wanasababu ya kutabasamu.
Aidha, amewataka wanafunzi waliopata ufadhili huo kujitahidi masomoni ili kuhakikisha kuwa wanapata matokeo bora huku mwakilishi wadi mteule katika bunge la kaunti ya Kilifi, Betty Sidi akimpongeza kiongozi huyo kwa kutekeleza shughuli hiyo kwa uwazi.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi wa wanafunzi waliopata ufadhili huo wakiongozwa na Ibrahim Matano, Sidi Chengo na Juma Kirao,
wamempongeza kiongozi huyo kwa kuendeleza haki na usawa, katika zoezi la ugavi wa basari hizo kwa wazazi wa wanafunzi hao, kinyume na hali ilivyokuwa awali.

