Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamaad Shariff Nassir amesema kuwa serikali ya kaunti hiyo, imeanza mikakati ya kuwakabili matapeli wanaoendeleza unyakuzi wa ardhi za umma kaunti hiyo.
Kwa mujibu wa gavana huyo ni kuwa wameanza harakati za kutafuta hatimiliki halali za ardhi hizo, ili kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa soko ambalo, huenda likawasaidia wakaazi wakaunti hiyo kujiendeleza kibiashara.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mardi wa Uvuvi na maendeleo ya kijamii na kiuchumi eneo la Liwatoni Mombasa, amesema kuwa sharti serikali hiyo irudhishe ardhi zote za umma, zilizo kuwa zimenyakuliwa na mabwenyenye.
Vile vile kiongozi huyo amesema kuwa sharti makundi ya usimamizi wa fuo za bahari BMU kaunti ya Mombasa, yabadilishwe na kuwa vyama vya ushirika, ili kusaidia katika kutafuta pesa za kuwapatia wavuvi vifaa vya kuendeleza shughuli zao za uvuvi, ili kukimu mahitaji yao kupita rasilimali ya bahari.
Kauli yake imeungwa mkono na Rais William Ruto, ambaye amesema kuwa hatua ya kubadilishwa kwa usimamizi huo kuwa vyama vya ushirika, kutasaidia pakubwa hatua ya wavuvi hao kujengwa uwezo, wa kutekeleza kazi zao kwa usatadi.

