Mwakilishi wa kamati ya uongozi wa shule ya msingi ya Central mjini Malindi kaunti ya Kilifi, Jokoleah Mugoi Mwamburi amesema shule hiyo ambayo iliafikia vigezo hitajika vya wizara ya elimu nchini kwa ajili ya masomo ya Sekondari Msingi, Junior Secondary inakabiliwa na changamoto za ukosefu wa madarasa, madawati na walimu wa kutosha.
Akizungumza na lulu Fm, Jokoleah amesema kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi, kunahitajika walimu wa kutosha ili kufanikisha mtaala wa elimu wa umilisi CBC na pia kuimarisha viwango vya elimu nchini.
Ni kauli ambayo imeungwa mkono na mwalimu mkuu wa shule hiyo Moses Masivahi Baraza na pia kutaja ukosefu wa maabara na maktaba kwenye shule hiyo ya Msingi ya Central Mjini Malindi kaunti ya Kilifi kuwa changamoto kuu katika kuwasomesha wanafunzi hao.
Aidha, Jokoleah ameiomba serikali kuingilia kati na kuweka mikakati thabiti ambayo itafanikisha vilivyo masomo ya sekondari Msingi kwenye shule ambazo ziliidhinishwa kufanikisha masomo hayo nchini.

