Naibu chifu wa wadi ya Shella eneo la Malindi kaunti ya Kilifi, Nichodemus Mwayele Ndundi, amesema wanaendeleza mikakati ya kuwakabili wanafunzi ambao wanatumia dawa za kulevya na pia kudhibiti visa vya mimba za utotoni mjini Malindi.
Katika mazungumzo ya kipekee na mwanahabari wetu baada ya kuandaa mkutano ambao uliwahusisha walimu na wazazi katika shule ya msingi ya Karima, Mwayele amesema kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo kuna baadhi ya wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wajawazito na pia wengine kuingia shuleni wakiwa wamebeba dawa za kulevya kama bangi.
Mwayele amesema wanafunzi ambao watapatikana wakiwa wamebeba bangi shuleni watakabiliwa kisheria.
Aidha, Mwayele amewataka wazazi wote katika wadi ya Shella eneo la Malindi kaunti ya Kilifi kuhakikisha watoto wao wanapelekwa shuleni na kuwataka kuwa karibu na watoto wao ili kuwalinda dhidi ya kupotoka kimaadili.
Vilevile, amesema wamekubaliana na wazazi kushirikiana na asasi husika kutoa ripoti na pia ushahidi ili wanaojihusisha na visa vya uhalifu mjini Malindi kaunti ya Kilifi wakabiliwe kisheria.

