Waziri wa elimu nchini Ezekiel Machogu anatarajiwa leo kutangaza rasmi matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE.
Kulingana na taarifa hafla ya kuyatangaza matokeo hayo imeratibiwa kuanza mwendo huu wa saa mbili asubuhi katika makao makuu ya baraza la kitaifa la mitihani KNEC jijini Nairobi.
Zoezi la kusahisisha ilitamatika wiki jana baada ya hapo awali kutatizika baada ya walimu waliokuwa wakisahisisha mitihani hiyo kushinikiza nyongeza ya marupurupu.
Aidha, walimu kadhaa waliokuwa wakishinikiza nyongeza hiyo waliondolewa huku usahishaji ukiendelea chini ya ulinzi mkali.
Jumla ya watahiniwa elfu mia nane themanini na wanane, mia mbili sitini na watatu ambao walifanya mtihani huo, miongoni mwao elfu mia nne ishirini, mia nane arubaini na watano ni wa Kike huku elfu mia nne na tano mia tisa sitini na wawili wakiwa wa kiume.
Huenda waziri Ezekiel Machogu akakosa kutangaza majina ya watahiniwa bora pamoja na shule walikosomea kama alivyofanya wakati wa kutangaza matokeo ya mtihani wa darasa la 8 KCPE.
Vilevile, Machogu anatarajiwa atakapokuwa anatangaza matokeo ya KCSE atazungumzia ufunguzi wa shule kwa muhula wa kwanza mwaka huu, kalenda ya masomo inaporejelewa baada ya kuathirika kuanzia mwaka wa mwaka wa 2020 kutokana na janga la virusi vya Corona.

