ATWAA SALIM MOHAMED ASHINDA KIPUTE CHA UWAKILISHI WA WADI YA SHELLA

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kaunti ya Lamu kupitia afisa wa IEBC eneo bunge la Lamu Magharibi Isaiah Saha imemtangaza Atwaa Salim Mohamed wa chama cha ODM kuwa mshindi kwenye kipute cha uchaguzi mdogo cha kuwania wadhifa wa uwakilishi wa wadi ya Shella Kisiwani Amu kaunti ya Lamu.
Kufikia jana saa nne unusu usiku masanduku yote ya kura kutoa vituo vyote 9 vya kupigia kura yaliweza kufika katika kituo cha kujumuisha kura cha Amu Fisheries kabla ya kujumuishwa na kuhesabiwa.
Atwaa Salim Mohamed alipata kura 1,053 huku mpinzani wake wa karibu Mohamed Hassan wa chama cha ANC akipata kura 573.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi Atwaa Salim Mohamed amewapongeza wenyeji wa Shella kwa kujitokeza na kumpigia kura kwenye kipute hicho.
Nao miongoni mwa wale waliokuwa kwenye kipute hicho wamesema uchaguzi huo uliandaliwa vyema kama ulivyokuwa umeratibiwa.
Wenyeji wa wadi ya Shella walipiga kura kumchagua mwakilishi wa wadi mpya baada ya kujiuzulu kwa Azhar Ali Mbarak ambaye kwa sasa ni spika wa bunge la kaunti ya Lamu.
Wadi hiyo yenye takribani wapiga kura 3,632 ni asilimia 47 pekee ya watu ambao walijitokeza kupiga kura.