WANANCHI WA WADI MBALIMBALI KAUNTI YA KILIFI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KWA WINGI KWENYE VIKAO VYA UMMA KUTOA MAONI

Mkurugenzi anayehusika na vikao vya umma vya kutoa maoni kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jamii kaunti ya Kilifi Mlewa Katana ameandaa kongamano na wenyeji pamoja wasimamizi wa maeneo wadi kaunti ya Kilifi.
Akizungumza na Lulu Fm baada ya kukamilisha mkutano huo ambao umefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Malindi kaunti ya Kilifi, Mlewa amesema lengo kuu limekuwa kuwapa fursa wananchi kuthibitisha mapendekezo yao waliyoyatoa hapo awali kwa wasimamizi wa maeneo wadi yao kuhusiana na utekelezaji wa miradi kaunti ya Kilifi ambayo yamechapishwa kwenye nakala za Mpango wa Maendeleo ya Kaunti.
Amesema kutakuwa na Kongamano lingine na wananchi tarehe 13 mwezi huu wa Disemba kwenye wadi mbalimbali kaunti ya Kilifi.
Amesema nakala za Mpango wa Maendeleo ya Kaunti (CIDP) ndizo zenye zinatoa mwongozo wa miradi yote yenye itatekelezwa na serikali ya kaunti ya Kilifi.
Kwa upande wake afisa wa miradi kutoka shirika linaloshughulikia amani na usalama la KECOSCE, Joseph Syanda ametoa wito kwa wenyeji wote kutoka wadi zote zilizoko kaunti ya Kilifi kujitokeza tarehe 13 mwezi huu wa Disemba kuthibitisha miradi ambayo walipendekeza ndio hiyo au la.