AMASON KINGI AMTAKA GAVANA GIDEON MUNG’ARO KUJITENGA NA MAANDAMANO

Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi amemtaka gavana wa kaunti ya Kilifi, Gideon Maitha Mung’aro kujitenga na masuala ya maandamano ambayo yamekuwa yakipangwa na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kufanyika kesho Jumatano.
Kulingana na Kingi licha ya gavana Mung’aro kuchaguliwa kupitia chama Cha ODM, anapaswa kuwa karibu na viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza Ili kunufaika na maendeleo.
Akizunguma katika eneo la Kamale wadi ya Adu katika eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi, Kingi amemtaka Mung’aro kushirikiana na serikali ya kitaifa ili wenyeji wa kaunti ya Kilifi wanufaike kupitia miradi mingi ya maendeleo kaunti ya Kilifi.
Kwa upande wake Gavana huyo ameeleza utayari wake katika kuhakikisha anashirikiana na spika huyo wa bunge la seneti, kwani yuko karibu na Rais wa William Samoei Ruto ili kupata suala la utata wa ardhi ulioko katika eneo hilo la Kamale na wadi ya Adu kwa jumla.