KAMISHNA WA KAUNTI YA LAMU AWATAKA WENYEJI KUWA NA SUBIRA

Kamishna wa kaunti ya Lamu Irungu Macharia amesema wenyeji wa kaunti hiyo wataendelea kusubiri kwa muda kabla ya kuruhusiwa kwa usafiri wa usiku kwenye barabara kuu ya Lamu – Witu – Garsen.
Macharia amesema wanaendelea kujadiliana na vitengo husika wakiwemo maafisa wa usalama pamoja na wamiliki magari ya uchukuzi wa umma ili kuona ni lini wataweza kuifungua barabara hiyo kwa ajili ya safari za usiku.
Hapo awali kabla ya barabara hiyo kufunguliwa kwa ajili ya usafiri wa mchana ilikuwa ni lazima magari yaliyokuwa yanatumia barabara hiyo mchana yasindikizwe na maafisa wa usalama hali iliyochangiwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa kundi la kigaidi la Al -Shabaab.