Serikali ya kaunti ya Kilifi imetakiwa kukamilisha miradi ya maendeleo iliyokosa kutekelezwa katika miaka ya hapo awali, licha ya serikali ya kaunti kuitengea fedha katika bajeti ya miaka iyopita, tangu kuanzishwa kwa ugatuzi.
Wakizungumza katika kikao cha Kilifi Citizen Forum ili kupendekeza miradi ya maendeleo katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2022/2023, wanaharakati wa kimaendeleo katika wadi mbalimbali eneo bunge la Kilifi Kusini kaunti ya Kilifi wamesema ipo miradi ambayo imekuwa ikikosa kutekelezwa katika eneo hilo, tangu mwaka 2015.
Wakiongozwa na Gladys Mwambui mkaazi wa wadi ya Mtepeni pamoja na Crispas Wanje mkaazi wa wadi ya Junju, wamedai wanasiasa wengi wamekuwa wakitekeleza maendeleo katika vijiji wanavyotoka na kutelekeza vijiji vingine katika wadi zao jambo ambalo, wanadai limechangia kutokamilika kwa miradi hiyo.
Aidha, Mwambui amependekeza kuboreshwa kwa huduma za afya katika taasisi za afya wadi Mtepeni huku Joseph Kuto akisisitiza haja ya wanasiasa, kutekeleza miradi inayopendekezwa na viongozi wao katika jamii, kwani wananchi ndio walio na ufahamu wa matatizo wanayopitia kauli ambayo imeungwa mkono na Eugene Mwarandu, mwaharakati wa wadi ya Shimo la Tewa ambaye ametaja umuhimu wa kukamilisha miradi ya barabara.
SERIKALI YA KAUNTI YA KILIFI YATAKIWA KUKAMILISHA MIRADI

