SERIKALI KUU YATAKIWA KUHARAKISHA UTOAJI WA MSAADA KWA WENYEJI WA TANA RIVER

Baadhi ya wawakilishi wa wadi kaunti ya Tana River wametoa wito kwa serikali ya kaunti hiyo na ile ya kitaifa kuharakisha utoaji wa msaada kwa wenyeji ambao wanaendelea kuathirika kutokana na hali ya ukame na baa la njaa.
Wawakilishi wa wadi hao Ismael Kodobo wa Hirimani, Mahmoud Ali wa wadi ya Sala na Maka Maimuna ambaye ni mwakilishi wa wadi mteule wanasema maeneo ya Bangale na Tana Kaskazini ndiyo ambayo yameathirika zaidi na ukame.
Wanasema idadi kubwa ya wenyeji wanahitaji msaada ili kuwanusuru kutokana na hali hiyo.
Akizungumzia suala hilo gavana wa kaunti hiyo Dhadho Godhana amesema wanashirikiana na mashirika mengine kuendelea kusambaza maji kwa wenyeji ili kukabiliana na kiangazi ambacho kimechangia kushuhudiwa kwa ukosefu wa maji.