RAIS MTEULE WILLIAM RUTO AWAPONGEZA WABUNGE NA MASENETA

Rais mteule William Ruto amewapongeza Wabunge na Maseneta walioungana kwa pamoja kuwachagua maspika wa mabunge yote mawili kwa kile alichosema kuwa wameonyesha kuwa na imani na muungano wa Kenya kwanza.
Kupitia mtandao wake wa twitter, Ruto ametoa pongezi hizo baada ya Moses Wetangula kushinda kwenye kura za kuchaguliwa kwa spika pamoja na naibu wake Gladys Boss.
Wetangula aliibuka mshindi kwa kupata kura 215 baada ya aliyekuwa mshindani wake wa karibu Kenneth Marende kupata kura 130.
Marende alijiondoa baada ya kufanyika kwa raundi ya kwanza ya uchaguzi hivyo Wetangula akatangazwa kuwa mshindi.
Akihutubia bunge hilo baada ya kutangazwa mshindi, Wetangula ameahidi kukuza imani ya umma katika uongozi wake sambamba na kufanikisha ushirikiano baina ya bunge la kitaifa na lile la seneti.