Waziri wa Afya Aden Duale ametoa onyo kali kwa vituo bandia vya afya, akisema kuwa hatasita kutoa orodha ya hospitali bandia, ambazo zilishiriki shughuli za ufisadi na iliyokuwa Hazina ya Kitaifa ya Afya (NHIF).
Aidha, waziri huyo ameazimia kutekeleza msako dhidi ya matabibu bandia, akitoa wito kwa wadau wote wa sekta ya Afya, kuhudumu kwa kuzingatia sheria.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika utekelezaji wa mpango wa Huduma za Afya kwa Wote (UHC).
Waziri huyo amezungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mkakati wa ushirikiano mpya, kati ya wizara ya Afya na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan.
Ushirikiano huo utapiga jeki matibabu ya operesheni, ikiwemo upandikizaji wa figo, oparesheni za moyo, kupitia Halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA). Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha Wakenya, wanapata huduma za dharura za Afya.
Waziri huyo ametoa wito kwa vituo vingine vya matibabu, vile vya umma na kibinafsi na vinanyomilikiwa na taasisi za kidni, kusaidia katika kuboresha shughuli za kutoa huduma za afya kwa wananchi.

