SPIKA WA BUNGE LA SENETI AMASON KINGI ATAKIWA KUTEKELEZA HAKI NA USAWA.

Spika wa bunge wa seneti nchini Amason Kingi, amewahakikishia viongozi wa bunge hilo haki na usawa, katika kuendeleza majukumu yake ndani ya bunge hilo.

Hii ni baada ya maseneta kulalamikia suala la spika huyo, kuegemea upande mmoja wakati anapofanya maamuzi, ama hata kuendesha vikao vya bunge hilo.

Akizungumza katika kikao maalumu cha viongozi wa bunge hilo, kinacho tarajiwa kutamatika hapo kesho kule Naivasha, Kingi amesema kuwa ufanisi wa bunge hilo, pia ni ufanisi wa serikali za kaunti humu nchini.

Kingi aidha amewataka viongozi wa bunge la seneti, ambao wanahudhuria kikao hicho, kuhakikisha kuwa wanatumia mda wao vyema katika kuzungumza masuala yatakayo saidia kuboresha shughuli za serikali za kaunti humu nchini.

Kwa upande wake kiongozi wa wengi kwenye bunge hilo Aaron Cheriyot, amelitaka bunge hilo kuwa na misimamo dhabiti, ambayo itasaidia katika kutatua changamoto zilizoko kwenye serikali za kaunti huku kiongozi wa wachache kwenye bunge hilo Stewart Madzayo, akikashifu hatua ya viongozi wa bunge hilo, kugharamikia safari zao jambo ambalo ni kinyume na sheria za bunge.