MLANGUZI WA DAWA ZA KULEVYA KIMATAIFA HELEN IKAREUT APATIKANA NCHINI UGANDA.

Maafisa wa Idara ya Upelelezi, DCI kwa ushirikiano na maafisa wa taifa jirani la Uganda, wamefanikiwa kumnasa mshukiwa mkuu wa biashara ya dawa za kulevya, kwa jina Helen Ikareut, raia wa Uganda.

Ikareut, ambaye ni mshirika mkubwa wa kusafirisha na kuuza dawa za kulevya katika ngazi za kimataifa, alikamatwa nchini Uganda na kusafirishwa humu nchini ili kujibu mashtaka dhidi yake, baada ya kuwa mafichoni kwa zaidi ya miaka miwili.

Msako dhidi ya Ikareut, ulianza Mei tarehe 18, mwaka wa 2023, wakati maafisa wa upelelezi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, waliponasa gramu elfu nne mia moja themanini na sita za bangi, zilizokuwa zimefichwa ndani ya katoni, hatua ambayo iliwapa maafisa hao mwelekeo wa kumfuatilia Ikareut, ambapo hatimaye maafisa wa Uganda walitambua

maficho yake nchini humo, na kumkamata, kisha kumkabidhi kwa maafisa wa humu nchini.

Ikareut alifikishwa katika Mahakama ya JKIA hapo jana na kushtakiwa kwa kosa la Usafirishaji wa Dawa za Kulevya.

Kesi dhidi yake itatajwa tena Agosti tarehe 25,mwaka huu.