TUME YA EACC YAONYWA DHIDI YA KUTUMIKA KISIASA NA SERIKALI.

Gavana wa kaunti ya Trans Nzoia, George Natembeya amemuonya mkurugenzi mkuu wa tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi nchini EACC, Abdi Ahmed Mohamud dhidi ya kukubali kutumika kisiasa na serikali ya kitaifa.

Kwa mujibu wa Natembeya tume hiyo inapaswa kutumia mamlaka yake katika kutekeleza haki na usawa dhidi ya wanasiasa wanao kamatwa na maafisa wa EACC kwa madai ya kushiriki ufisadi katika afisi za umma.

Akihutubia wananchi katika kaunti hiyo, Natembeya ameibua madai ya maafisa wa EACC kupewa masharti ya kumhangaisha kwani hakuwa na makosa yeyote.

Natembeya ameelezea kuwa na haki ya kukosoa serikali kwa mujibu wa sheria za taifa hili huku akiwataka wananchi kumuungan mkono katika juhudi zake za kupinga serikali ya kitaifa.

Haya yanajiri siku chache baada ya Natembeya kukamatwa kwa madai ya utumizi mbaya wa afisi na kufanya biashara na wawekezaji walipewa zabuni na serikali ya kaunti yake.