Waziri wa fedha John Mbadi, amefichua kuwa uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kusitisha ufadhili kwa Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID), utasababisha upungufu wa shilinghi bilioni 52, katika Mwaka wa kifedha wa 2024/25 kwa taifa hili.
Mbadi ambaye alikifika mbele ya bunge la Seneti, ameeleza kuwa sekta zilizoathiriwa ni pamoja na afya, utawala, elimu na usalama wa chakula.
Katika uchanganuzi wake, shilingi bilioni 2.8, zingewekezwa katika sekta ya elimu, ili kutoa mafunzo kwa walimu, usaidizi kwa taasisi za TVET, ufadhili wa masomo, ujenzi wa madarasa ya awali katika shule za msingi za umma na kusaidia vyuo vikuu humu nchini.
Sekta ya utawala ingepokea shilingi bilioni 1.1, kuimarisha uwezo wa kitaasisi, kusaidia elimu inayoendelea ya wapigakura kwa uchaguzi wa 2027, kukabiliana na visa vya magenge ya kiuhalifu katika kaunti za Pwani na kuunga mkono juhudi za serikali.
USAID pia ingetoa shilingi bilioni 16.5, kwa ajili ya usalama wa chakula, ili kukabiliana na baa la njaa katika maeneo kame, kutoa msaada wa chakula kwa wakimbizi wa Dadaab na Kakuma, na kuwekeza katika vyama vya ushirika na mbinu za teknolojia.
Waziri Mbadi amesema kuwa usaidizi wa USAID, hauhesabiwi katika bajeti lakini unatoa usaidizi wa ziada.
Ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa fedha, serikali kuu, itafanya mabadiliko kwenye bajeti iliyopo, ili kuweka kipaumbele masuala muhimu..
Mbadi ametaja umuhimu wa hatua za muda mrefu kubuniwa ikiwa ni pamoja na Kenya kujitegemea kupitia uchumi unaostawi.
Hii itahusisha kuimarisha mabadiliko ya kilimo, kusaidia biashara ndogo ndogo, ndogo na za kati na za kidijitali pamoja na ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

