AFISI YA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI NANCY GATHUGHU ASEMA KUNA WAFANYAKAZI HEWA KATIKA BAADHI YA KAUNTI.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, imefichua kuwa Kaunti nane nchini ziliajiri maelfu ya wafanyakazi bila kufuata sheria katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024,
Kulingana na ripoti hiyo, wafanyakazi hao waliajiriwa pasi na nafasi za ajira kutangazwa, kupitia vyombo vya habari wala hakuna mahojiano yaliyo fanywa ili kuwapiga msasa.

Taarifa hiyo katika ripoti iliyotolewa wiki jana, inaonyesha kuwa wafanyakazi hao, walioajiriwa katika kaunti za Samburu, Trans Nzoia, Nairobi, Narok, Nandi, Embu, Machakos na Uasin Gishu, wanaendelea kulipwa mamilioni ya fedha, kama mishahara na marupurupu kila mwezi.

Ripoti hiyo vile vile, inaonyesha kuwa katika kaunti zingine, hakukuwa na ushahidi kuwa nafasi wazi za ajira zilikuwepo, kabla ya wafanyakazi wapya kuajiriwa.
Na katika kaunti zingine, faili zenye maelezo kuhusu uajiri wa wafanyakazi wapya hazikuwepo.

Wafanyakazi walioajiriwa kwa njia hiyo isiyozingatia sheria ni pamoja na maafisa wa usimamizi, walimu wa chekechea, makarani, wakurugenzi wa idara mbalimbali, maafisa wa ustawi wa kibiashara na maafisa wa kitengo cha usalama.

Kwa mfano, katika Kaunti ya Samburu, serikali hiyo iliajiri watu 29, kufanya kazi katika Kitengo cha Utekelezaji Miradi katika Afisi ya Gavana, bila idhini kutoka kwa Bodi ya Uajiri wa Watumishi wa Umma katika Kaunti (CPSB).

Ndani ya kipindi hicho cha ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma katika kaunti, hamna rekodi kuhusu matangazo ya nafasi za kazi, uorodheshaji wao baada ya mchujo, mahojiano na uteuzi kamili ziliwasilishwa kwa wakaguzi.