Wahudumu wa afya katika kaunti ya lamu wametoa makataa ya siku saba kwa serikali ya kaunti ya Lamu, wakiitaka kushughulikia changamoto zote wanazopitia la sivyo watasusia kazi hadi pale matakwa yao yatakapo shughulikiwa.
Aidha wamesema kuwa wanapitia changamoto nyingi katika kazi yao, hivyo kuitaka serikali ya Kaunti ya Lamu kuwaskiliza na kutekeleza wajibu wake.
Wahudumu hao vilevile wamesema kuwa viongozi katika serikali hiyo, wamekuwa wakinyamazia matatizo wanayopitia licha yao kuyawasilisha kwao.
Kulingana na wahudumu hao kati ya changamoto wanazopitia ni kucheleweshwa kwa mishahara, maeneo duni ya utendakazi, kupokea vitisho kutoka kwa baadhi ya wafanyikazi wa serikali ya kaunti miongoni mwa maswala mengine.

