WAZIRI JUSTINE MUTURI AKOSOA HATUA YA SERIKALI KUU KUDAI HAINA UFAHAMU KUHUSIANA NA WALIOKO VIJANA WALIOTEKWANYARA.

Waziri wa utumishi wa umma nchini Justin Bedan Njoka Muturi, ameisuta serikali ya kitaifa kutokana na ongezeko la idadi ya visa vya vijana wa taifa hili kutekwa nyara na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi.

Kulingana na waziri Njoka, idadi kubwa ya familia zimeendelea kukabiliwa na hali ya msongo wa mawazo, kutokana na kutoweka wa wanao katika hali tatanishi na hakuna taarifa zozote ambazo, jamii hizo zimekuwa zikipokea kutokana na visa hivyo.

Katika taarifa yake kwa wanaandishi wa habari, Muturi amesema kuwa kama mmoja wa wazazi walio na watoto ambao wamewahi kutekwa nyara, hajawahi kupokea sababu zozote zilizochangia mwanawe Leslie Muturi ,kutoweka katika hali tatanishi miezi sita iliyopita, licha yake kuhudumu kwenye serikali ya Kenya kwanza na katika kamati ya kitaifa ya usalama, wakati wa tukio hilo.

Muturi ameikashifu serikali kuu kwa madai ya kutokuwa na ufahamu kuhusiana na walioko vijana ambao bado hawaja achiliwa huru, baada ya wao kutekwa nyara huku akisema kuwa huenda hatua hiyo, ikachangia serikali kuendeleza uongozi wa kiimla kinyume cha sheria.

Aidha, mda mfupi baada ya taarifa ya Muturi kwa vyombo vya habari hapo jana, Idara ya Upelelezi nchini Kenya DCI, ilichapisha taarifa huku ikishikilia kuwa kesi inayohusu kutekwa nyara kwa mwanawe Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi, ingali inaendelezwa na uchunguzi kamili wa kisa hicho, umekuwa ukiendelezwa kwa mwendo wa kinyonga, kwani mtoto wa waziri huyo pekee, ndiye aliyerekodi taarifa.