WAVUVI ENEO LA MALINDI KAUNTI YA KILIFI WALALAMIKIA UHABA WA SAMAKI BAHARINI.

Wavuvi eneo la Malindi kaunti ya Kilifi wamelalamikia kupungua kwa idadi ya samaki, katika fuo za bahari zilizoko eneo hili la Malindi.

Kulingana na wavuvi hao wakiongozwa na Kahindi Kadenge, Paul Charo pamoja na Grace Neema, ambaye ni muuzaji wa samaki wa kukaranga wamesema wamekuwa wakivua samaki, chini ya kiasi cha kilo mbili kila wanapoenda baharini kuvua samaki.

Wakizungumza na wanahabari eneo hili la Malindi wamesema kuwa hatua hiyo imeathiri pakubwa mapato yao, kutokana na ongezeko la gharama ya maisha licha ya wao kuongeza pia bei ya samaki sokoni.

Kauli hizo zimeungwa mkono na mwenyekiti wa usimamizi wa fuo za bahari eneo la Shella hapa mjini Malindi Yunus Aboud, ambaye ametaja suala la baadhi ya wavuvi kutoka mataifa mengine kuvua samaki, wakitumia meli kubwa kama chanzo cha kushuhudiwa kwa suala hilo.

Aidha wavuvi hao sasa wanapendeleza serikali ya kauinti pamoja na ile ya kitaifa, kuwasaidia kupata vifaa vya kisasa ili kutekeleza shughuli zao za uvuvi, kama wavuvi wengine wa mataifa jirani.