Rangers wapaa Bandari wakizuiwa kusonga KPL

Posta Rangers ndiyo timu iliyoimarika zaidi kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya kulipua washiriki wapya Kisumu All Stars 3-0 ugani Machakos katika mechi ya raundi ya tano Jumatatu na kuruka juu nafasi saba hadi nambari tano.

Mabingwa watetezi Gor Mahia wanasalia kileleni kwa alama 12 baada ya kuandikisha ushindi wa nne mfululizo walipokung’uta Zoo 1-0 Jumapili.

Wanabenki wa KCB na wanamvinyo Tusker wako juu katika nafasi ya tatu na tano baada ya kulima Nzoia Sugar 1-0 na Kakamega Homeboyz 3-1, mtawalia.

Vijana wa hapa Pwani Bandari FC wanasalia nafasi ya saba wakiwa na alama nane ndani ya mechi tano walizocheza ambapo wameshinda mara mbili, kutoka sare mara mbili pamoja na kupoteza mtanange mmoja.

KCB sasa inashikilia nafasi ya pili kwa alama 10 ikizidia Tusker ubora wa magoli.

Western Stima, ambayo ilikabwa 0-0 na wanajeshi wa Ulinzi Stars, imepisha KCB na Tusker na kutulia katika nafasi ya tatu kwa alama tisa.

Rangers, ambayo haikuwa imepata ushindi katika mechi tatu, imekalia nafasi ya tano kwa alama nane, sawa na Ulinzi na Bandari zinazofuatana katika nafasi ya sita na saba mtawalia. Bandari ilizabwa 2-1 na Sofapaka mnamo Jumapili.

AFC Leopards, ambayo haikuwa na mechi wikendi, imeteremka kutoka nafasi ya tatu hadi nambari nane.

Klabu hiyo maarufu kama ‘Ingwe’ ina alama saba.

Inatofautiana na Sofapaka, Homeboyz na Mathare United kwa ubora wa magoli tu.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

SUBSCRIBE TO OUR E- NEWSLETTER

Subscribe to our mailing list and get interesting stuff and updates to your email inbox.