Ozil kujaza pengo DC United

Viongozi wa klabu ya DC United ya Marekani wamemtaka kiungo Mesut Ozil kukubali mshahara mdogo kujiunga na miamba hao wa Major League Soccer (MLS) wanaopania kulijaza pengo la Wayne Rooney.

Ozil kwa sasa ndiye mchezaji wa pili baada ya Alexis Sanchez wa Manchester United anayedumishwa kwa mshahara wa juu zaidi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Nyota huyu wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ujerumani kwa sasa hutia mfukoni kima cha Sh46 milioni kwa wiki. Ukubwa wa gharama ya kumdumisha Ozil uwanjani Emirates ni kiini cha usimamizi wa Arsenal kutaka kuagana naye, na tayari mawakala wake wamefichua kuhusu mpango wa kutua jijini Washington kuanzisha mazungumzo na DC United kuhusu uwezekano wa kumsajili.

Kiini cha DC United kuyahemea maarifa ya Ozil ni kujaza nafasi ya Rooney ambaye kwa sasa anajiandaa kuanza majukumu ya kuwa kocha na mchezaji wa Derby County mnamo Januari 2020.

Hata hivyo, huenda fedha zikawa kikwazo kikubwa katika jitihada za Ozil kubanduka kambini mwa Arsenal ambao watalazimika kugharimia sehemu kubwa ya mshahara wa nyota huyu.

Tayari Kuondoka kwa Rooney kambini mwa DC United ni afueni kubwa kwa kikosi hicho ambacho kimekuwa kikimpokeza mshahara wa hadi Sh11 milioni kwa wiki.

Kwa sasa, ina maana kwamba Ozil anapokezwa mshahara ambao ni mara tatu zaidi kuliko ule ambao mchezaji ghali zaidi katika MLS hutia kapuni mwishoni mwa kila wiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

SUBSCRIBE TO OUR E- NEWSLETTER

Subscribe to our mailing list and get interesting stuff and updates to your email inbox.