ALEX KAZUNGU, DHAHABU INAYOIPA THAMANI YOUNG BULLS

Mshambulizi hatari Alex Kazungu wa Young Bulls – klabu ambayo inacheza mitanange ya ligi la daraja la kwanza kitaifa la (FKF) kutoka hapa pwani – anazidi kuonyesha kiu yake ya mabao zaidi kwani hadi kufikia sasa amefunga magoli kumi msimu huu wa mwaka 2020/2021.

Young Bulls ambayo ni klabu iliyo katika nafasi ya nne katika jedwali la daraja la kwanza la kitaifa iliititiga Liberty Sports Club ya Nairobi wikendi iliyipita ambapo Alex Kazungu aliweka kimyani mabao mawili katika mtanange huo.

Tama la Spoti lilimzukia mshambulizi huyo mazoezini katika uwanja wa Alaskan mjini Malindi na kufanya mahojiano naye na kwenye suala la jinsi anavyozidi kufunga magoli katika mechi nyingi alisema, “Mkufunzi wetu bwana Billy Mwangemi hutuambia kila siku tufike mazoezini saa tisa mchana ila mimi hurauka saa moja kabla masaa hayo peke yangu kufanya mazoezi yangu binafsi. Mimi natilia maanani sana kasi yangu katika mchezo kwa kukimbia uwanjani ili kuzoesha misuli yangu na mapafu. Nahakikisha kuwa napiga mikwaju nikiwa na wenzangu uwanjani. Lakini cha msingi kama mchezaji mshambulizi huwa nazingatia sana kasi yangu na hii ndio siri ya mafanikio ya mabao niliyofunga msimu huu.”

Na kwenye suala la labda anamfuatilia sana mchezaji gani ughaibuni anayempa motisha wa kufanya jitihada zaidi alisema haya, “Kylian Mbappe ndiye mchezaji ambaye namfuatilia sana huko ughaibuni anayechezea timu ya Ufaransa na klabu ya Paris Saint Germain. Napenda sana anavyocheza, kasi yake, nguvu zake na bidii yake. Mimi huwa ninapakua na kutazama video zake anavyocheza alafu nikiingia uwanjani ninafanya. Na pia hujaribu kufanya nilichotazama kwenye video hizo nikiingia dimani ila kikubwa Zaidi ambacho hata mkufunzi wetu hutusisitizia ni kuwa tuwe na nidhamu uwanjani. Ningependa kuhimiza vijana wenzangu wajitokeze tukuze vipaji bila kufa moyo kwani aijuaye kesho ni mwenyezi Mungu tu kwani ipo siku jitihada zetu zitalipa na mataifa wajue kuwa Kilifi kuna talanta.”

Young Bulls wikendi hii watasafiri hadi mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kuchuana na Balaji EPZ na mkufunzi Bill Mwangemi amesema wanamatumaini makubwa kushinda mchuano huo.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

SUBSCRIBE TO OUR E- NEWSLETTER

Subscribe to our mailing list and get interesting stuff and updates to your email inbox.