Mbwembwe za AFCON | Mbinu 3 zilizoilaza Tanzania mikononi mwa Kenya

Watanzania hawaamini kilichotokea katika mechi yao dhidi ya jirani zao Kenya. Ulikuwa mchezo wa kufurahisha na kusisimua; Taifa Stars ya Tanzania kuongoza katika kipindi cha kwanza na baada ya dakika tisini, wakaachwa hoi bila pointi tatu walizopigania.

Ilikuaje Kenya ikaipiku Tanzania?

1. Mikakati

Wakufunzi wa Kenya kwa muda wamekuwa wakilaumiwa kwa kutokuwa na mikakati ya kutosha wanapounga kikosi pamoja na kufanya mabadiliko mabovu wakati mechi inapoendelea.

Kuanzia Reinhard Fabisch, Jacob ‘Ghost’ Mulee na hata kocha wa sasa mfaransa Sébastien Migné.

Kabla ya kikosi cha Kenya kuelekea Misri, Migné alilaumiwa kwa kuwaacha wachezaji wenye uzoefu kama mshambuliaji matata Allan Wanga na badala yake kumbeba Paul Were licha ya kuwa alikuwa anauguza jeraha.

Kufuatia kupoteza mechi 2-0 dhidi ya Algeria, kocha Migne aliwachezesha Johanna Omollo, David Owino and Eric Ouma na kuwapumzisha Eric Johanna, Philemon Otieno na Dennis Odhiambo.

Katika mechi dhidi ya Taifa Stars, baada ya Tanzania kufunga, alimwondoa mchezaji wa safu ya kati Francis Kahata na kumuingiza John Avire aliyesababaisha ikabu iliyopeleka Kenya kupata bao la kwanza kando na kunoa makali ya safu ya ushambulizi.

Hii ilibadilisha mizani na kuifanya Tanzania kuwa na wakati mgumu kuudhibiti mpira haswa katikati mwa uwanja ili kufanya mashambulizi.

2Uwekezaji kwenye timu

Serikali ya Kenya imekuwa ikilaumiwa na mashabiki wa soka nchini kwa kutowekeza kwenye michezo vya kutosha katika timu ya taifa.

Wakati wa kufuzu kwa kipute hiki, serikali ilidai haina fedha za kutosha kuwalipa marupurupu wachezaji waliokuwa wakielekea kupambana na Ethiopia.

Hata hivyo serikali ilibadili mkondo mara timu ilipofuzu.

Rais wa shirikisho la kandanda nchini Kenya (FKF) Nick Mwenda alidai kuwa wachezaji wote kwenye kikosi wangepokea anagalau Ksh 767, 550.00 kila mmoja kama marururupu.

Pamoja na hayo,aliongezea kuwa kila mchezaji angepokea Ksh 255, 850.00 kwa kila mechi watakayoshinda.

Haya kwa sasa fanya hesabu tu!

Kwa jumla serikali ilikuwa imetenga Ksh 255, 850,000.00 kuisadia timu ya Harambee Stars kujitayarisha katika michuano ya Afcon.

Pesa hizo zilitumika kukituma kikosi hicho Ufarasa walikomenyana na Madagascar na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Bila shaka matayarisho hayo yaliyowezeshwa na fedha kuliwapa vijana wa Stars motisha zaidi.

3.Historia

Historia huwa sehemu kubwa sana ya soka. Kila mara mashabiki hukumbushana na kijitanua vifua kwa mahasidi wakimbushana ushindi wa jadi.

Mashabiki huenda wakasahau kumlipa mtu deni ama hata kuoga lakini si siku timu yao iliposhinda kombe fulani ama kumshinda hasimu wao mkubwa.

Na hapa pia historia ilirudiliwa. Harambee Stars na Taifa Stars zilikuwa zimekutana mara 48 kabla ya mechi ya hiyo.

Na kwa mechi hiyo, Kenya ilikuwa imevuna ushindi zaidi. Kwa mechi hizo 48, Kenya ilikuwa imeishinda Tanzania mara 23 (47.9%), kutoka sare mechi 10 (20.8%) na kupoteza mechi 15 (31.3%).

Timu hizi mbili zilikutana mwanzo tarehe 25 Septemba 1971 na mechi hiyo ikaishia sare ya 1-1.

Hata hivyo timu hizi haziachani mbali katika msimamo wa FIFA kwani Tanzania ilikuwa nafasi ya 134 na na kenya 130 ikiwa ni utofauti wa hatua nne tu, kabla ya mechi ya juzi. Kwa mashabiki wengi wa nchini Kenya, watasema, ukivuliwa chutama. Raundi hii walimvua Taifa Stars.

Kwenda Mbele itakuaje?

Ushindani kati ya Tanzania na Kenya utazidi kuwepo. Wanavyitana wenyewe kama ‘mashemeji’ ina maana wana uhusiano ambao hauvunjiki hivi karibuni.

Kunao watu maarufu tu ambao wameoa hapa nchini Kenya huku wakenya wengine wenye majina makubwa wakiwa pia wao wameoa na kuolewa Tanzania. Zaidi ni uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili.

Mechi ya makundi ya kombe la AFCON inaendelea. Kenya watapambana na Senegal siku ya Jumatatu 1 Julai, wote wakiwa na pointi tatu inagawaje Kenya ina uzuri wa mabao.

Tanzania watakutana na Algeria, ambao ndio viongozi wa kundi C kujaribu kuvuna pointi tatu. Watashikilia imani kuwa Watamshinda kwa mabao mengi wakiamini Senegal atamchapa Kenya ili warudi wote Afrika Mashariki.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

SUBSCRIBE TO OUR E- NEWSLETTER

Subscribe to our mailing list and get interesting stuff and updates to your email inbox.