MANDZUKIC ATUA AC MILAN

Vinara wa ligi kuu ya Italia (Serie A), AC Milan wamejinasia huduma za fowadi matata raia wa Croatia, Mario Mandzukic bila ada yoyote.

Kwa mujibu wa mkataba wa nyota huyo, Milan watakuwa radhi kurefusha muda wa kuhudumu kwa Mandzukic uwanjani San Siro kwa mwaka mmoja zaidi baada ya kandarasi ya sasa kutamatika mwishoni mwa msimu huu.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Juventus na Bayern Munich hajakuwa na klabu tangu aagane rasmi na kikosi cha Al Duhail kinachojivunia kwa sasa maarifa ya fowadi wa Harambee Stars ya Kenya, Michael Olunga.

Akiwa Bayern, Mandzukic aliwaongoza miamba hao wa soka ya Ujerumani kutia kapuni taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2013 kabla ya kuongoza Juventus kunyanyua mataji manne ya Serie A kati ya 2015 na 2019. Mandzukic amewahi pia kudhibiti mikoba ya Atletico Madrid.

Alifungia Croatia bao la pili katika kichapo cha 4-2 walichopokezwa na Ufaransa kwenye fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi.

“Nimefurahi sana kusikia ujio wa Mandzukic. Sasa tutakuwa wakongwe wawili tegemeo kambini mwa Milan na wapinzani wataumia sana,” akasema fowadi matata wa Milan, Zlatan Ibrahimovic, 39.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

SUBSCRIBE TO OUR E- NEWSLETTER

Subscribe to our mailing list and get interesting stuff and updates to your email inbox.