Kilifi | Wakaazi wa Kadzuhoni wapokea msaada baada ya makaazi yao kubomolewa

Wakazi wa Kadzuhoni kaunti ndogo ya Magarini katika Kaunti ya Kilifi wamepokea msaada kutoka kwa mashirika mbalimbali ya kijamii hapa Pwani kwa ushirikiano na kituo hiki cha Lulu Fm baada ya makazi yao kubomolewa mapema mwezi huu wa Julai.

Akizungumza na wakazi wa eneo hilo hapo jana wakati wa kuwakabidhi vyakula na nguo miongoni mwa vitu vingine Mkurugenzi wa majanga katika Kaunti ya Kilifi Joshua Malingi amesema kwamba watasimama na wananchi walioathirika katika ubomozi huo.

Malingi pia amewapongeza wananchi na mashirika ya kijamii kwa kuungana na kitengo cha majanga katika kuwasaidia waathiriwa.

Kwa upande wao wananchi wameeleza kufurahishwa kwao na misaada wanayopata inayowasaidia kuendelea na maisha yao huku wakiomba msaada zaidi wa malazi sawia na sare za shule kwa watoto wao.

Ikumbukwe mapema mwezi huu katika mahojiano ya kipekee na kituo hiki mwakilishi wa wadi ya Gongoni Albert Kiraga alisema tayari baadhi ya viongozi kaunti ya Kilifi waliwasilisha ombi katika mahakama kuu mjini Malindi ili kusitisha ubomozi kwenye ardhi hiyo yenye utata ya Kadzuhoni eneo bunge hilo la Magarini.

Kiraga alisema kuwa viongozi wa Kaunti ya Kilifi akiwemo Gavana Amason Kingi na Mbunge wa Magarini Michael Kingi waliwasilisha ombi hilo mbele ya mahakama ya Malindi hadi pale rufaa ya uamuzi uliotolewa na mahakama kuhusiana na utata unaoizingira ardhi hiyo itakapo sikilizwa.

Kiraga alidokeza kuwa Mahakama ilikuwa imetoa agizo la wakazi walio kwenye Kipande hicho cha ardhi kuondoka baada ya kusikiliza kesi iliyokuwa imewasilishwa mahakamani kuhusiana na mgogoro huo, uamuzi ambao Kiraga alisema uliegeamea upande wa bwenyenye kufuatia kuchelewa kwa ushahidi kutoka upande wa wakaazi.

Aidha Kiraga amekanusha madai kuwa viongozi wa kaunti ya Kilifi walikuwa wamelinyamazia swala hilo kabla ya ubomozi huo na kusema kuwa viongozi wa eneo hilo walihusika tangu mwanzoni mwa utata huo.

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

SUBSCRIBE TO OUR E- NEWSLETTER

Subscribe to our mailing list and get interesting stuff and updates to your email inbox.