Je, Chelsea ndio mabingwa msimu huu?

Klabu ya Chelsea watashuka dimbani American Express leo usiku kumenyana na Brighton katika mchuano wa ligi kuu Uingereza, EPL, utakaomshuhudia kocha Frank Lampard akitegemea zaidi silaha mpya alizojinasia muhula huu.

Chini ya ukufunzi wa mwanasoka wa zamani klabu hiyo ya darajani Frank Lampard, Chelsea wametumia zaidi ya Sh35 bilioni hadi kufikia sasa msimu huu ili kusajili wachezaji wapya ambao wanatazamiwa kutikisa uthabiti wa Liverpool na Manchester City katika soka ya Uingereza.

Kufikia sasa, Chelsea wamesajili wanasoka watano wapya akiwemo beki matata mzawa wa Brazil, Thiago Silva aliyeagana na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa bila ada yoyote.

Silva, 35, alitia saini mkataba wa mwaka mmoja na Chelsea ambao watakuwa na fursa ya kurefusha zaidi kipindi cha kuhudumu kwa nyota huyo ugani Stamford Bridge kutegemea matokeo yake msimu ujao.

Aliyekuwa beki wa Nice, Malng Sarr, beki wa kushoto Ben Chilwell aliyebanduka Leicester City, fowadi Hakim Ziyech aliyetokea Ajax, Kai Havertz raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 21 aliyetokea Bayer Leverkusen na mshambuliaji Timo Werner ambaye alikatiza uhusiano wake na RB Leipzig ndio wanasoka wengine waliosajiliwa na Chelsea hivi majuzi.

Hata hivyo, gazeti la Evening Standard limefichua kwamba Sarr atatumwa kwa mkopo katika mojawapo ya klabu za EPL ili ajiimarishe zaidi katika msimu wa 2020-21.

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Chelsea, Lampard aliyetegemea sana huduma za chipukizi, alichochea waajiri wake kumaliza kampeni za EPL katika nafasi ya nne, kutinga hatua ya 16-bora ya UEFA na kufika fainali ya Kombe la FA mnamo 2019-20.

Lampard amefichua pia maazimio ya kujinasia huduma za kipa atakayekuwa kizibo cha Kepa Arrizabalaga anayetazamiwa kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Sevilla au Atletico Madrid.

Andre Onana wa Ajax, Jan Oblak wa Atletico na Nick Pope wa Burnley ni miongoni mwa makipa wanaoviziwa sasa na Chelsea baada ya Yann Sommer wa Borussia Monchengladbach, Dean Henderson wa Manchester United na Roman Burki wa Borussia Dortmund kutia saini mikataba mipya kambini mwa waajiri wao.

Moto wa usajili ambao klabu ya Chelsea umewasha umetajwa kusababishwa na kufungiwa kusajili wachezaji msimu uliopita ila hatuwezi weka kando swala la kwamba Lampard anawania kutuzwa ubungwa wa EPL.

Sadfa iliyopo ni kwamba Chelsea inaanza msimu kwa kucheza siku ya Jumatatu siku ambayo msimu wa 2014/2015 na 2016/2017 ilianza kama hivyo na ikashinda mataji ya EPL.

Katika siku ya kwanza ya kampeni za EPL msimu huu wa 2020-21, Arsenal waliwatandika Fulham 3-0, Liverpool wakatolewa jasho na Leeds United kabla ya hatimaye kuwapiga limbukeni hao 4-3 ugani Anfield nao Crystal Palace wakawapokeza Southampton kichapo cha 1-0 uwanjani Selhurst Park. Newcastle United waliwapiga West Ham United ya kocha David Moyes 2-0 katika London Stadium.

Wacha katambe sasa! Mshindi tutamjua tu.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

SUBSCRIBE TO OUR E- NEWSLETTER

Subscribe to our mailing list and get interesting stuff and updates to your email inbox.