Mutindika awataka wazazi kuchukua jukumu la malezi kikamilifu

Kamati ya usalama kaunti ya Kilifi imewalaumu wazazi kwa kutelekeza majukumu yao katika ulezi wa watoto wa Kike.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Magu Mutindika anasema wazazi wengi wamekosa kukidhi mahitaji ya watoto hao ikiwamo kuwanunulia sodo jambo ambalo limewafanya wengi kutafuta mbinu mbadala za kujikimu na hatimaye kuishia kwenye mimba za mapema.

Akizungumza mjini Kilifi, Mutindika ametaja utepetevu wa maadili ambao unapaswa kufundishwa watoto hao tangu wakiwa wadogo ndio chanzo kikuu cha mimba za mapema .

Mutindika ameeleza kushangazwa na jinsi ambavyo wazazi wengi hupenda kuwatuma watoto wa kike nyakati za usiku akisema wakati huo ndio muda ambao hukutana na majanga hayo ya mimba za mapema.

“Wazazi wengi hawataki kushuhulikia watoto wao wa kike, na hakuna kulaumu serikali ya kaunti au ya kitaifa kwa mambo na mimba za mapema, kwani alipata mimba akiwa nyumbani? Saa tatu mtoto wako yuko nje hujui yuko wapi anafanya nini aliko? Haya mambo ni jukumu la mzazi ndio suluhu la yote” Alisema Mutindika.

Tayari serikali ya kitaifa chini ya wizara ya usalama wa ndani Daktari Fred Matiang’i ilipiga marufuku Disco Matanga baada ya kudaiwa kuchangia mimba za mapema kaunti ya Kilifi.

Mapema mwaka jana gavana wa kaunti ya Kilifi Amason Jefa Kingi alipendekeza wabunge wa kitaifa kupasisha sheria itakayodhibiti janga la mimba za mapema ikiwamo kuhasiwa kwa mwanamume yeyote atakayepatikana akijihusisha na mapenzi na watoto wadogo.

Takwimu za hivi punde kutoka wizara ya vijana, jinsia na utamaduni kaunti ya Kilifi zilinakili kuongezeka kwa kesi za Mimba za mapema kutoka elfu kumi na tatu hadi elfu kumi na saba baada ya idara hiyo kufanya upekuzi zaidi katika maeneo ya Matsangoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

SUBSCRIBE TO OUR E- NEWSLETTER

Subscribe to our mailing list and get interesting stuff and updates to your email inbox.