Viongozi Liverpool, mabingwa watetezi Manchester City na Chelsea waliendeleza nyanyaso zao dhidi ya waonyonge Sheffield United, Everton na Brighton kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambayo imeingia raundi ya saba, wikendi.
Liverpool iliwachapa Sheffield United goli moja kwa nunge, Mancity ikilima Everton magoli matatu kwa moja huku Chelsea ikiandikisha ushindi wa magoli mawili bila jawabu dhidi ya Brighton.
Aston Villa walitoka sare ya magoli 2-2 dhidi ya Burnley, Bournemouth ikiandikisha matokeo sawia ya hayo baina ya West Ham United huku Crystal Palace ikishinda magoli mawili kwa nunge dhidi ya Norwich.
Watford ikiwa ugenini walilimwa 2-0 dhidi ya Wolves wakati Tottenham ikiandikisha ushindi wa 2-1 dhidi ya Southampton.
Aidha Leicester walinyeshea mvua ya magoli matano bila jawabu Newcastle United huku ngarambe inayongojewa kwa hamu na gamu ya wageni Arsenal wakimenyana na Manchester United dimbani Old Trafford ikitarajiwa kupigwa leo Jumatatu saa nne usiku saa za Afrika Mashariki.