HABARI

MTU MMOJA KATI YA KUNDI LA WATU KUMI ANAUGUA MATATIZO YA KIAKILI

 

MTU mmoja kati ya kundi la watu kumi anaugua matatizo ya kiakili humu nchini tangia chimbuko la janga la Corona.

Ni kauli yake wizara ya afya inayoongozwa na waziri Mutahi Kagwe ambaye alikiri hayo jana kuwa tangia chimbuko la janga hilo visa vya matatizo ya kiakili vimekithiri mno huku akisema kuna haja ya visa hivyo kuangaziwa hata zaidi.

Kagwe amesema kuwa shirika la afya duniani WHO limeorodhesha Kenya kuwa nambari 29 ulimwenguni katika mataifa ambayo yana idadi ya juu zaidi ya watu wanaojitoa uhai.

Waziri Kagwe amesema kuwa idadi kubwa ya watu wamekumbwa na msongo wa mawazo miongoni mwa matatizo mengine ya kiakili huku chanzo kikuu cha matatizo hayo ya kiakili yakitajwa kusababishwa na ubugiaji wa pombe kupita kiasi.

Waziri huyo amesema kuwa vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 29 ndio waraibu zaidi wa pombe kulingana na ripoti ya utafiti wa kiafya iliyotolewa.

Waziri Kagwe amewataka wananchi kutohusisha matatizo ya kiakili na dhana potovu wala kuendekeza unyanyapaa kwa wale wanaougua matatizo ya kiakili.

Aidha jopokazi lililokamilisha ripoti ya utafiti huo limependekeza kubuniwe tume itakayopewa jukumu la kukabiliana na maswala ya matatizo ya kiakili miongoni mwa mikakati mingine.

 

JINSIA YA KIUME YAENDELEA KUANDIKISHA IDADI KUBWA YA MAAMBUKIZI YA COVID-19

Jumla ya watu 8,250 wameambukizwa virusi vya Corona baada ya wengine 183 kuripotiwa kuambukizwa virusi hivyo saa 24 zilizopita.

Akitoa tathmini za kila siku kuhusiana na maambukizi ya virusi hivyo,waziri wa afya, Mutahi Kagwe amesema kuwa 177 kati ya 183 hao ni wakenya huku 6 wakiwa wa mataifa ya kigeni.

119  ni wanaume na 64 ni wa jinsia ya kike huku kaunti ya Nairobi ikirekodi visa 100 mombasa ikirekodi visa 13.

Kagwe amesema kuwa watu wengine 90 wameripotiwa kupona ugonjwa wa covid- 19 idadi kamili ya waliopona ikifikia watu 2,504 huku watu watatu wakipoteza maisha idadi kamili ya waliopoteza maisha ikifikia 187.

Waziri Kagwe amewataka wakenya kufuata maagizo ya serikali pasipo kungoja kushurutishwa na idara polisi kwani serikali haikufungua mipaka kwa sababu imedhibiti virusi vya korona bali kwa sababu za kuimarisha uchumi.

KUFUNGULIWA KWA SAFARI ZA NDEGE KUNAENDELEA KUIBUA HISIA MSETO

 

Katibu mkuu wa baraza la walimu wa Madrassa ukanda wa pwani,Ustadh Athman Said amesema kuwa agizo la serikali la kuruhusu ndege za kimataifa kuanzia safari zake mwezi Agosti huenda likapelekea ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona mjini Malindi na nchini kwa jumla.
Ustadh Said amesema kuwa wakaazi wa Malindi wapo katika hatari ya kupata maambukizi hayo ikizingatiwa kwamba mji wa Malindi ni miongoni mwa miji ya kitalii ambayo watalii wengi wa ughaibuni huzuru mji huu.
Kwa upande wake mwanaharakati wa maswala ya kijamii,Shariffa Ali amesema kuwa ni sharti serikali iweke mikakati dhabiti ya kuhakikisha kuwa wageni wote wanaozuru taifa hili wanapimwa ili kubaini iwapo wameambukizwa virusi vya korona au la.

SUBSCRIBE TO OUR E- NEWSLETTER

Subscribe to our mailing list and get interesting stuff and updates to your email inbox.